Ijumaa 23 Oktoba 2026 - 08:30
Ikhlasi Katika Matendo na Kuwafuata Ahlul-Bayt (as) Ndio Njia ya Kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu

Hawza/ Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Ardabil Iran, huku akieleza hatua za safari ya kiroho na malezi ya nafsi amesema kuwa; ikhlasi katika matendo, kumfuata Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt (as), pamoja na kujiepusha na mazingira yaliyochafuliwa na madhambi, ni miongoni mwa mambo muhimu yanayomwezesha mwanadamu kujikurubisha na Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza mjini Tehran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Amili, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Ardabil na Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Ardabil, alisema hayo siku ya jana Alhamisi alipokuwa akishiriki katika kipindi cha televisheni cha Samt-e Khoda (Upande wa Mwenyezi Mungu). Katika maelezo yake kuhusu hatua za safari ya kiroho na malezi ya nafsi, alisisitiza kuwa ikhlasi katika matendo, kumfuata mwanadamu mkamilifu na kujiepusha na uchafu wa kimaadili na kiroho ni miongoni mwa mambo muhimu yanayomwezesha mwanadamu kufanikiwa katika njia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Akieleza kuwa kufikia daraja la tauhidi na kumtambua Mwenyezi Mungu ni safari ya hatua kwa hatua inayohitaji juhudi na mapambano dhidi ya matamanio ya nafsi, alisema: “Qur’ani Tukufu imeeleza njia na siri mbalimbali za kumwezesha mwanadamu kufanikiwa katika safari hii. Hivyo, mwanadamu anapaswa kuyatekeleza mafundisho hayo hatua kwa hatua, ili aweze kuimarisha uwezo wake wa kiroho.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Amili, akizungumzia tofauti kati ya utambuzi wa mwanadamu kupitia hisia za nje na utambuzi wa kiroho, alisema: “Mbali na macho na masikio ya nje, mwanadamu pia amejaliwa uwezo wa kiroho. Anapoendelea kukua kiroho, upeo mpya wa maarifa hufunguka mbele yake, na hivyo kuweza kufikia maarifa yanayovuka mipaka ya utambuzi wa kawaida.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Ardabil, huku akisisitiza umuhimu wa kueneza irfani inayotegemea Qur’ani na madhehebu ya Ahlul-Bayt (as), alitoa tahadhari kwamba kiu ya mwanadamu ya kumtambua Mwenyezi Mungu na kufikia maarifa ya kiroho wakati mwingine hutumiwa vibaya na makundi potovu. Kwa hiyo, alisema, Hawza zina wajibu wa kufafanua njia sahihi ya irfani na safari ya kiroho kwa mujibu wa Qur’ani na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), ili watu wasifuate mikondo isiyo sahihi.

Aliitaja ikhlasi katika matendo kuwa ni hatua ya kwanza katika safari ya kiroho, akirejelea msisitizo wa Qur’ani Tukufu kuhusu kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa unyoofu na ikhlasi, alisema: “Mwanadamu anapaswa kutanguliza radhi za Mwenyezi Mungu katika maamuzi na matendo yake kuliko maslahi binafsi, kutafuta kuwavutia watu au misukumo ya kimaada, ikhlasi huwa na maana ya kweli pale mwanadamu anapozingatia radhi za Mwenyezi Mungu hata katika nia na misukumo yake ya ndani kabisa.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Amili, akirejelea riwaya zinazozungumzia thawabu za matendo yanayofanywa kwa ikhlasi, alibainisha kuwa thamani ya tendo hutegemea nia ya mtu. Wakati mwingine, tendo dogo linaweza kuwa na thamani kubwa sana iwapo litafanywa kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu pekee. Jambo muhimu ni kwamba mwanadamu, badala ya kutafuta nafasi na heshima mbele ya macho ya watu, anapaswa kuzifanya radhi za Mwenyezi Mungu kuwa kipimo cha matendo yake.

Aliongeza kuwa mojawapo ya njia za kuvuta rehema na neema za Mwenyezi Mungu ni kuwasaidia watu walioko katika matatizo na wenye mahitaji. Mwanadamu hapaswi kusita kufanya matendo mema kwa ajili ya wengine, kwa sababu kuwahudumia waja wa Mwenyezi Mungu kuna athari kubwa katika maisha yake ya kiroho.

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Ardabil aliashitia pia kumfuata mwanadamu mkamilifu kuwa ni hatua nyingine katika safari ya kiroho, akasema: “Mtu anayetaka kusonga mbele katika njia ya kiroho anapaswa kuyalinganisha maisha yake, mwenendo wake, maamuzi yake na mahusiano yake na mifano mitukufu ya Mwenyezi Mungu pamoja na mafundisho ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt (as).

Haiwezekani kudai kuwa unawafuata watu hawa watukufu, huku katika matendo yako ukifuata njia tofauti na ile waliyoipitia.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Amili, akisisitiza umuhimu wa kuufuata mwenendo wa Ahlul-Bayt (as), alieleza wazi kuwa mafundisho ya Qur’ani na Ahlul-Bayt (as) hayafungwi katika zama au kipindi maalumu, bali mifano hii mitukufu inaendelea kuwa mwongozo kwa watu wa nyakati zote. Alisema kuwa ili mwanadamu apate maarifa sahihi, anapaswa kupima maisha na mwenendo wake kwa kuzingatia vigezo hivyo.

Katika kuendelea na maelezo yake, aliashiria kujiepusha na mazingira na mikusanyiko inayochochea madhambi na kudhoofisha imani za kidini kuwa ni miongoni mwa mahitaji mengine muhimu ya safari ya kiroho. Alisema: “Mwanadamu anapaswa kuwa makini na mazingira anayoishi pamoja na watu anaoshirikiana nao, kwa sababu baadhi ya mienendo na mahusiano ya karibu huathiri hatua kwa hatua roho na utu wa mwanadamu, na si rahisi kujitenga na athari zake mbaya mara zinapojengeka.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Amili, akirejelea mafundisho ya Qur’ani Tukufu kuhusu kujiepusha na mikusanyiko ambapo hukumu na aya za Mwenyezi Mungu zinadhihakiwa, alisema: “Muumini hapaswi kubaki bila kujali mbele ya kuvunjiwa heshima matukufu ya dini na kudhoofishwa tunu za kidini. Kushikamana na itikadi hakumaanishi kuzikubali kwa maneno pekee, bali kunahitaji kuwajibika na kutetea tunu ambazo mwanadamu amezikubali na kuziamini.”

Akisisitiza kuwa kujiepusha na mazingira yaliyochafuliwa hakumaanishi kukatisha mahusiano yote ya kijamii, aliongeza: “Mwanadamu anapaswa kuwa makini katika mahusiano yake na kujiepusha na kuhudhuria bila ulazima katika mazingira yanayoweza kusababisha kudhoofika kwa hali yake ya kiroho na imani zake za kidini. Kwa kufanya hivyo, ataandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kukua na kuimarika kiroho.”

Mwisho, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Ardabil, akirejelea riwaya kutoka kwa Bibi Fatima Zahra (s.a.) kuhusu kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi, alielezea matumaini yake kwamba wanadamu wataimarisha ikhlasi zao na kufuata mafundisho ya Qur’ani na Ahlul-Bayt (as), ili waweze kuifuata kwa usahihi njia ya utumwa kwa Mwenyezi Mungu na safari ya kiroho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha